SWAHILI MEDIA GROUP USA (MMK)-TUMETIMIZA SIKU TISINI !

TUMETIMIZA SIKU TISINISasa tunafikisha miezi mitatu tangu tuanzishe rasmi TV ,Blog na Radio online, kwa binadamu ni siku chache maana hata kutambaa atakuwa bado, kwa chombo cha habari  itategemea na uanzishwaji na wadau wake wanachukuliaje.

Kwa upande wetu tunachukulia bado tunakuwa, hivyo  tunamshukuru Mungu na wadau wetu  kwa siku hizi chache ambazo tumekuwa  hewani.

"Ni Jambo la kujivunia kwamba mmethubutu", tunanukuu maneno ya Waziri mkuu mstaafu mheshimiwa Edward Lowassa, aliyotueleza tulipofanya mahojiano naye hapa mjini Washington DC.  Tunaipokea kauli yake kwa unyenyekevu mkubwa na kama changamoto Kwetu sisi,wamiliki na wafanyakazi wote wa Swahili.

Ukubwa na nguvu ya chombo chochote cha habari unatokana na wadau ambao ndio wasikilizaji na wasomaji wake, nasi tunafurahia sana ushirikiano ambao Tumekuwa tukiupata kutoka kwenu nyinyi wadau wetu, tunapenda kusema hili kwa kudhamiria wasomaji na wasikilizaji wa Swahili Kwetu sisi nyinyi ni familia.

Tunapenda kuweka wazi kuwa bila ushirikiano wenu tusingeweza kufanya haya tunayoyafanya, licha ya muda huu mfupi tumeweza kufanikiwa kusogeza radio yako kwa karibu zaidi kwani sasa unaweza kusikiliza Swahili Radio kwenye simu yako ya kiganja (cell phone).

Katika kipindi hiki pia tumekuwa tukiwasiliana na wadau wetu ambao ni DCTV ili watukubalie show zetu tunazozalisha Kwao tuweze kuzionyesha kwenye online na pia Radio yetu iwe inasikika kwenye radio za kawaida hapa Marekani na Tanzania, tuko kwenye hatua za mwisho za kufanikisha hayo. Pia mikataba mbalimbali imeshafanywa ili kuanzia Novemba mpate vipindi mbalimbali na kwa muda maalum.

Tunawashukuru pia washiriki wetu VOA, BBC na Radio Umoja wa mataifa kwa  kushirikiana nasi na kukubali Swahili kurusha matangazo yao, hivyo kuanzia mwezi Novemba wadau wetu mtaweza kupata taarifa  za habari na vipindi mbalimbali kutoa katika radio hizo za kimataifa kupitia Swahili mtandaoni na kwenye simu za viganja.

Katika wingi kuna mengi,unapokuwa kwenye kusanyiko lolote lile kukwaruzana kupo, nasi kwa kutambua hilo, tunajua kuna sehemu nyingine tumekwaruza, tunapenda kusema samahani pale tulipokwaruza mtu au watu, kama waumgwana tunarudia kusema samahani na wale waliotukwaruza tumewasamehe, tunapofikisha siku  hizi tisini, Mbiu yetu ni "tufungue ukurasa mpya kwa maendeleo ya wote".
Tunakaribisha maoni na ushauri wenu, kama tulivyosema awali, nguvu yetu ni nyinyi wadau wetu, hiki ni chombo chenu, tunaahidi kuwa jicho, sikio na mdomo wa jamii, bila woga tutaripoti kwa nia ya kuhabarihisha, elimisha na kuburudisha lakini hatutotekwa na kiburi wala majivuno au woga, tunaahidi kuwa chombo huru cha habari lakini kinachojali maadili.

Pia tunakaribisha mtu yeyote anayependa kutoa ushauri au  kuhabarihisha ajisikie huru kuwasiliana nasi kwa email ya swahilimediausa@gmail.com, nasi tunaahidi kuwasiliana naye au kufanyia kazi ushauri wake au kupokea habari yake.
Kila siku ya ijumaa Swahili Blog itakuwa inatoa TAHARIRI.