CHAMA CHA MAPINDUZI- CCM.
TAWI LA UINGEREZA.
W: www.ccmuk.org E: info@ccmuk.org
Tel: +44 740 558 1 668 / +44 740 486 3333.
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi TAWI la Uingereza, wanapenda kuungana na Wanachama wenzao Tanzania na popote pale walipo duniani katika kusherehekea miaka 36 ya kuzaliwa na kushika hatamu kwa Chama Chetu cha Mapinduzi.
Kwa furaha tumekuwa pamoja kimawazo tukifuatilia kwa ukaribu maadhimisho ya kitaifa ya sherehe za Miaka 36 yaliyofanyika kwenye Mkoa wa Kigoma na Kufikia kilele chake Leo Jumanne. Ni dhahiri na tumeshuhudia maelfu ya Wana-Kigoma na Watanzania wote kwa ujumla walijitokeza kwa wingi katika kuadhimisha siku hii, yote haya yanaonyesha mapenzi ya Watanzania kwa Chama Cha Mapinduzi.
Wana CCM UK tunatambua ya kuwa Chama Cha Mapinduzi tumefika hapa tulipo kutokana na jitihada za kimapinduzi za waasisi wetu na waazilishi wa vyama vya TANU na ASP , chini ya Uongozi wa Baba Wa Taifa - Marehemu Mwalimu Julius K Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume . CCM hii ya leo imesimama imara kama matunda ya hekima na busara za wazee wetu na kuona mbali kwa kuvunja vyama vya TANU na ASP kwa taadhima kubwa na kuunda Chama kimoja madhubuti cha Siasa nchini Tanzania . Miaka 36 baadae CCM imeendelea kutunza umoja, amani na upendo ,kwa kurithi yale waliyoaacha wazee wetu. Tunawashukuru sana na kuwaombea Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema peponi.
Wana CCM-UK , Tunapenda kutoa pongezi na shukrani zetu kwa Viongozi wetu wote wa CCM waliopita kwa kusimamia na kuingoza nchi chini ya CCM na kuweza kudumisha amani , upendo na umoja wa ndani na nje ya Tanzania. Tanzania ,chini ya Chama Cha Mapinduzi ilikuwa katika mstari wa mbele katika kuikomboa Afrika , na kushirikiana na wenzetu wa nchi nyingine za Afrika kisiasa na kijamii, hususani katika Umoja wetu wa nchi za Afrika Mashariki.
Wana CCM-UK ,Tunapenda tutoa pongezi za dhati na za pekee kwa Uongozi wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wetu Dr. Jakaya Mrisho Kikwete , katika kuiongoza nchi kwa upendo, amani na utulivu. Pongezi zetu zaidi kwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na viongozi wake, katika kutekeleza sera za CCM kupitia Ilani za Uchaguzi za Mwaka 2005 na 2010. Nchi yetu imepiga hatua kubwa sana kimaendelea chini ya CCM na Tunatambua na kupongeza maendeleo nchini Tanzania yaliyotokana na Sera za CCM.
Ni jamabo la kujivunia sana kwa Wana- CCM hususani katika kipindi hiki kigumu chenye changamoto ambazo zimeikumba dunia nzima katika hali ya kiuchumi na mabadiliko ya kisiasa,kuona kwamba CCM imeweza kusimama madhubuti na imara na kuendelea kuongoza Nchi kwa amani. Licha ya changamoto zinazojitokeza mara nyingine, kubwa na la msingi tunawapongeza sana Viongozi wetu na wananchi wa Tanzania kwa kuendelea kusimamamia na kudumisha hali ya utulivu, amani na upendo miongoni mwa Watanzania wote ndani na nje ya nchi.
Wana –CCM UK tunajivunia hali ya CCM kushirikiana pamoja na Vyama vingine vya siasa ndani ya Tanzania kwa nia na lengo la kuiletea maendeleo nchi yetu . Hii inadhihirisha ukomavu wa Demokrasia wa hali ya juu na CCM imekuwa ni mfano wa kuigwa na vyama vingi vya siasa barani Afrika , na vilevile vyama vya siasa nchini Tanzania.
Wana CCM –UK na Dispora kwa ujumla,tunaendelea kushukuru kwa busara na hekima za mwenyekiti wetu wa CCM Dr.Jakaya M Kikwete, kwa kuwezesha matawi ya chama tawala nje ya nchi kufanya kazi, hili limewapa nafasi wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi na Watanzania waishio nje ya nchi kuweza kupata nafasi ya kuchangia maendeleo na yale mazuri tuliyojifunza nje katika nyanja za kisiasa na kiuchumi na kurudisha nyumbani kwa manufaa ya nchi yetu kwa ujumla.
Kwa Watanzania wenzetu , wana ccm wenzetu ,tunawashukuru wote na tunaomba tuendelee kudumisha amani ,upendo,na utulivu wetu ambao umekuwa ni ngao na ni sifa ya Tanzania popote uendapo duniani. Bila ya Chama Cha Mapinduzi , Tanzania ingekuwa wapi ?
Happy Birthday Chama Cha Mapinduzi
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania.
Imetolewa na Idara ya Itikadi, Siasa na Uenezi
CHAMA CHA MAPINDUZI TAWI LA UINGEREZA.