MASTAA WA BONGO; NANI MSHIRIKINA, NANI SI MSHIRIKINA?

                             HABARI HII KUTOKA GLOBAL PUBLISHERS

SIKATAI kuwa kuna uchawi au wachawi na ushirikina au washirikina. Pia sibishi kuwa kuna ulimwengu wa giza kwani hata vitabu vitakatifu vinasema kwamba kulikuwa na uchawi, wachawi, ushirikina na washirikina. Kama wewe ni msomaji wa vitabu hivyo, unakumbuka enzi za Musa katika Biblia kwenye Agano la Kale?
Mbali na vitabu vitakatifu, mara kadhaa tumesikia habari za wenzetu walioendelea kuwa mambo hayo yapo na yanafanyika.
Turudi nyumbani Bongo. Katika habari zilizovuta hisia za wengi wiki iliyopita ni sakata la uchawi na ushirikina kutajwa mara nyingi zaidi katika ulimwengu wa mastaa wa Kibongo.
Nitakupa hadidu za rejea za listi ya mastaa wa Kibongo waliowahi kulalamikia ishu hiyo halafu nitafungua mjadala huru ambao utalenga kutafuta majibu sahihi ya ushirikina katika sanaa ya Kitanzania.
Huko nyuma mastaa kadhaa waliwahi kulalamika kuwa kuna watu wanawaloga. Mfalme wa TAKEU, Nice Lucas Mkenda aliwahi kulalamikiwa na mwigizaji Miriam Jolwa ‘Jini Kabula’ kuwa anamloga kipindi kile wakiwa na uhusiano wa kimapenzi. Swali; alikuwa anamloga ili iweje?
Mara kadhaa lejendari wa Bongo Fleva, Aboubakar Katwila ‘Q-Chillah’ amekuwa akilalamika kulogwa, huko nyuma aliwahi kukaririwa akisema kuwa alilogwa na lejendari mwenzake, Khaleed Mohamed ‘TID’. Wiki iliyopita aliibuka tena na kudai kuwa kuna msanii wa muziki huo anatumia nyota yake kufanya vizuri kwenye gemu, madai ambayo yalielekezwa kwa jamaa anayeng’ara kwa sasa, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Tukimwacha Chillah, sakata lingine linamhusu Diamond ambapo jamaa mmoja aitwaye Ustadhi Yahya Michael hivi karibuni aliibuka na kudai kuwa yeye ndiye mganga wa msanii huyo na amekuwa akimsaidia kwa muda mrefu ili kumfanya awe na mvuto na kuwa juu kimuziki huku staa huyo akishindwa kukanusha au kufafanua uhusiano wake na jamaa huyo.
Alipoulizwa msanii mwenzake, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ kuwa yeye na Diamond wamekuwa wakihusishwa na ushirikina katika muziki alikataa katakata akidai kuwa hajui chochote.
Baadaye TID naye alifunguka kuwa siyo siri kwamba aina ya muziki wanaoufanya umejaa ushirikina na kwa sasa si jambo la siri.
Itakumbukwa mwaka jana, prodyuza mkubwa ambaye ni bosi wa Studio na Lebo ya Bongo Records, Paul Khalfan Matthysse ‘P-Funk’ au Majani, naye alikiri muziki wa Bongo Fleva kujaa vitendo vya kishirikina bila kutaja nani anamloga nani na kwa malengo gani.
Bila kumsahau Rehema Chalamila ‘Ray C’ ambaye kwa sasa hasikiki kutokana na matatizo ya kiafya, mara kadhaa aliwahi kukaririwa akidai kwamba anahisi kuna mtu anamloga.
Tukiacha upande wa muziki, kwenye filamu za Kibongo, huko ndiyo hali ni mbaya kabisa. Baadhi ya wasanii wamekuwa wakitajwa kujihusisha na masuala hayo waziwazi.
Mwaka jana, mama wa Wema Sepetu, Mariam Sepetu alikaririwa na kituo kimoja cha runinga akidai kuwa mwanaye (Wema) ameharibikiwa kwa sababu ya kufanyiwa mambo ya kishirikina na marafiki zake ndiyo maana mambo yake yanavurugika. Hata hivyo, hakuwataja marafiki hao lakini alikiri mwanaye kuhusishwa na mambo ya kishirikina.
Nakumbuka wakati ndoa yake na Hamad Ndikumana ikiingia kwenye mgogoro mzito na kuvunjika, Irene Uwoya alikaririwa akisema kuwa kuvurugika kwa mambo yake kulitokana na kulogwa na msanii mwenzake ambaye hakumtaja.
Huku nyuma, mastaa wa maigizo wa kitambo, Blandina Chagula ‘Johari’ na Nuru Nassor ‘Nora’ waliwahi kutamka wazi kuwa wanalogwa na wanawajua watu wanaowafanyia hivyo.
Nimetoa mifano hiyo michache kutoka kwenye Bongo Fleva na filamu lakini ukweli ni kwamba katika bendi za dansi nchini, hali ni mbaya zaidi. Kuna bendi ambayo hata uwalipe mabosi wake kiasi gani cha fedha hawawezi kukubali kufanya shoo katika ukumbi fulani kwa madai kuwa kuna bendi nyingine imefukia uchawi ukumbini hapo hivyo hawatapata watu.
Mifano hiyo inatupa picha halisi ya wasanii wetu kuwa hawaamini katika juhudi binafsi bali wanategemea nguvu za ndumba.
Baadhi yao wanajaribu kutafuta visingizo baada ya kuchuja kwenye gemu na muda wao kuwatupa mkono.
Wengine wameabudu bangi na madawa ya kulevya na katika kutafuta mchawi wakajikuta wakisingizia wamelogwa. Ipo mifano mingi. Jiulize nani anakuloga? Kwa nini anakuloga? Acheni kutafuta mchawi kwani kama wewe si mshirikina huwezi kuamini mambo ya kishirikina. For the love of game!

***DMK BLOG INA SWALI *** JE UTAJUAJE FULANI MCHAWI KAMA WEWE SIO MCHAWI??