MWANAMUZIKI RAY C - AMTEMBELEA RAIS KIKWETE IKULU KUMPA AHSANTE !


Mwanamuziki wa Kizazi Kipya Rehema Chalamila maarufu kama RAY C akimshukuru Rais Kikwete kwa kumsaidia matibabu,alipomtembelea Ikulu jijini Dar es Salaam leo.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa pamoja na Ray C wa kwanza kushoto ni Mama yake mzazi Ray C Bibi Margareth Mtweve (kushoto) na kulia ni Sarah Mtweve Dada yake Ray C. Picha na mdau Freddy Maro wa Ikulu

Msanii wa Kizazi Kipya hapa nchini ,maarufu kama Bongo Flavour, Bi Rehema Chalamila anaejulikana zaidi kama Ray C, leo mchana amefika Ikulu ya Dar-Es-Salaam kumshukuru Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa msaada mkubwa wa matibabu yake ambayo yanafanyika jijini Dar-Es-Salaam chini ya uangalizi maalum.
Ray Camefika Ikulu akiongozana na mama yake mzazi Bibi Margareth Mtweve ambaye pia amemshukuru Rais Kikwete kwa msaada huo mkubwa ambao umesaidia kurudisha hali ya kawaida ya Ray C.
Rais amempongeza Ray C kwa kukubali hali yake ya kiafya na hatimaye kukubali kupata matibabu ambayo bado anaendelea nayo chini ya uangalizi maalum.
Rais amemtaka mwanamuziki huyo kufuata masharti ya madaktari ili aweze kupona kabisa na hatimaye kurudia hali yake ya mwanzo na kurejea katika shughuli zake za kujitafutia kipato na maisha.
Kwa vile Ray C bado yuko katika matibabu, hatutaweka wazi sehemu anayotibiwa hadi atakapokuwa tayari kabisa kurudi katika shughuli zake rasmi hivyo tunaomba jamii impe ushirikiano huo na kuheshimu taratibu zake za matibabu ili hatimaye aweze kupona kikamilifu.

Imetolewa na :
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu-DSM
10 Desemba, 2012