Vyama vya siasa vinaweza kufanya kazi pamoja na kuleta mabadiliko - Maalim Seif


Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Kigogo Dar es Salaam jana 
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Kigogo Dar es Salaam jana 
Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kinondoni Juma Nkumbi akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Kigogo Dar es Salaam jana 
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akimtwisha ndoo ya maji mwananchi wa mtaa wa “Msisiri B” baada ya kufungua rasmi kisima cha maji katika mtaa huo. (Picha na Salmin Said, OMKR).

Na Hassan Hamad OMKR 
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema vyama vya siasa vinaweza kufanya kazi pamoja na kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo. 

Amesema kitu cha msingi ni kwa vyama hivyo kuwa na nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi.
Maalim Seif ameeleza hayo kwa nyakati tofauti wakati akiwa katika ziara ziara ya siku moja ya kutembelea miradi ya maendeleo katika manispaa ya Kinondoni mjini Dar es Salaam, ambapo baade alifanya mkutano wa hadhara katika eneo la Kigogo. Amesema suala la vyama vya siasa kushirikiana katika kuendesha nchi sio jambo geni na kutolea mfano kwa nchi zilizoendelea zikiwemo za Ulaya.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amefahamisha kuwa muda mfupi tangu kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar imepata mafanikio makubwa ambayo hayakuweza kupatikana kabla ya kuwepo kwa muundo huo wa serikali.

Ameyataja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kuwawezesha wakulima wa zao la karafuu kupata hadi asilimia 80 ya soko la dunia, kuongezwa mishahara ya wafanya kazi kwa asilimia 25, pamoja na kupunguza bei ya pembejeo za kilimo.


Kabla ya kufanya mkutano wa hadhara, Maalim Seif alifungua kisima cha maji safi na salama katika mtaa wa Msisiri kata ya Mwananyamala, kufungua Ofisi ya serikali ya mtaa wa Bwawani, pamoja na kufungua ofisi ya serikali ya mtaa wa Mtambani.

Akizungumzia kuhusu sera za Chama hicho Maalim Seif amesema lengo lao ni kuwatumikia wananchi ili waweze kupata haki zao kama inavyoeleza ilani ya chama hicho.

Amesema CUF kinakusudia kuendeleza Umoja wa Kitaifa, na kwamba iwapo watapata ridhaa ya kuongoza nchi mwaka 2015, chama hicho kitaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa pande zote mbili za Muungano.

Kuhusu raslimali za Taifa Maalim Seif amesema bado hazijatumika ipasavyo kuwanufaisha wananchi, ambapo amesema Chama hicho kitaweka sera maalum ya kuhakikisha kuwa Watanzania wananufaika kikamilifu na rasilimali za nchi yao.

Ameelezea umuhimu wa kuzingatia matumizi ya rasilimali watu ambayo imetumiwa na nchi zilizoendelea kuleta mabadiliko katika nchi zao.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara Bw. Julius Mtatiro amesema mchakato wa kuundwa kwa katiba mpya ya Tanzania ni changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi ili iwe fursa kwa Watanzania.

Amesema bila ya kuwepo na uwazi katika katiba, ujanja na ufisadi utaendelea kukithiri na kuzorotesha maendeleo ya nchi.

Nao wananchi wa kata za Mwananyamala na Mtambani wameelezea matumaini yao ya upatikanaji wa huduma bora katika mitaa yao baada ya kuibuka kwa miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ya maji safi na salama pamoja na kuimarika kwa majengo ya serikali za mitaa.